Aliyeongoza maandamano ya kumng'oa Rais azungumza

Alhamisi , 11th Apr , 2019

Mwanaharakati, Alaa Salah (22) wa Sudan aliyeongoza maandamano ya kumtoa madarakani Rais wa nchi hiyo, Omar Al-Bashir ameonyesha furaha ya matunda ya kazi waliyoanza kuifanya tangu Jumatatu kwa kusema Bashir ameondoka.

Alaa Salah

Salah amejizolea umaarufu kwa picha yake ambayo amesimama juu ya gari katikati ya watu kusambaa sehemu nyingi ulimwenguni akitambulika kama shujaa kwa taifa hilo.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Salah ameandika kwamba, "Al-Bashir ameondoka, tumefanikiwa", ikiwa ni saa moja tangu Jeshi kuwaweka chini ya ulinzi viongozi waandamizi wa serikali ya Al - Bashir.

Ameongeza kwamba "Wanawake wa Sudan wamekuwa wakishiriki katika mapinduzi nchini. Ikiwa utaona historia ya Sudan, wasichana wetu wote wameongoza. Ni sehemu ya urithi wetu. Ninafurahi sana kushiriki katika mapinduzi haya na ninafurahi mapinduzi yetu yamefikia lengo lake la kwanza".

Mapema leo, kabla ya Shirika la Habari nchini Sudan kuhabarisha kwamba Jeshi la nchi hiyo linatarajia kutangaza taarifa muhimu juu ya mustakabali wa nchi, Salah aliweka wazi kwamba amekuwa akipokea vitisho vya kuuliwa baada ya picha na video zake kusambaa.

"Nimekuwa nikipokea vitisho vya kifo baada ya picha yangu & kusambaa . Sitamtukuza. Sauti yangu haiwezi kufutwa.  Al-Bashir atawajibika ikiwa kitu chochote kitatokea kwangu," Salah.

Maandamano dhidi ya Bashir yalianza toka mwezi Disemba ambapo awali maandano yalianza kwa kupinga kupanda kwa bei ya vyakula lakini yamekuwa makubwa na kubadili lengo na kutaka kumng'oa rais madarakani.

Mpaka sasa Waziri Mstaafu wa Ulinzi, Abd al-Rahim Hussein na Waziri wa Ulinzi Awad Ibn Awaf wameripotiwa kukamatwa.

Salah ni mwanafunzi wa Chuo cha Kimataifa cha Sudan ambapo anasomea Uhandisi na usanifu.