Arusha: Mmoja afariki dunia, baada ya soko kuungua

Jumapili , 29th Mar , 2020

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP Koka Moita, amesema kuwa mfanyabiashara mmoja amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Mount Meru, baada ya kupata mshituko alipogundua kuwa vibanda vyake vyote vya biashara vimeteketea kwa moto.

Mabaki ya vibanda baada ya soko la Samunge Arusha, kuteketea kwa moto.

Tukio la kuteketea kwa soko la Samunge mkoani Arusha, limetokea usiku wa kuamkia leo Machi 29, 2020, ambapo hadi sasa chanzo cha moto huo bado hakijajulikana, ambapo pia idadi ya vibanda vilivyoteketea na moto pia bado haijajulikana.

"Wakati zoezi la kuzima moto linaendelea mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la James Peter Chemba (57), alipofika kwenye eneo la tukio alikuta vibanda vyake vimeungua na kupata mshituko na kuzimia na alikimbizwa hospitali ya Mount Meru, ambapo alifariki wakati akipatiwa matibabu" amesema ACP Koka.

Aidha Kamanda Moita amesema kuwa uchunguzi wa kubaini hasara ya mali zilizoungua unaendelea.