'Asilimia 85 ya watu wana uono hafifu' - Dkt Frank

Jumatano , 9th Oct , 2019

Shirika la Afya Dunia (WHO), limeweka mpango mkakati wa kuhakikisha wanawake wanapewa kipaumbele cha kupatiwa matibabu ya afya ya macho, ambapo takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 55 wana upungufu wa kati wa kuona.

Vipimo vya macho

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 9, 2019 na Rais wa Chama cha Madaktari wa Macho nchini Dkt Frank Sandi, ikiwa ni katika kuelekea wiki ya Afya ya macho Duniani, inayoadhimishwa kila Alhamisi ya pili ya mwezi Oktoba, ambayo kwa mwaka huu imeangukia Oktoba 10, 2019.

''Takribani watu bilioni 1.3, wanakadiriwa kuwa na upungufu wa kuona na asilimia 85 wanaishi katika nchi zenye kipato cha chini, ikiwemo nchi ya Tanzania'' amesema Dkt Sandi.

Kwa upande wake Makamu Rais wa Chama hicho Dkt Cyprian Ntomoka, amesema kuwa watu wengi wamekuwa wakitafuta huduma ya macho yao, wakiwa wamechelewa hali inayopelekea kuwa na idadi kubwa ya watu wenye matatizo hayo.

''Watu wengi wanaishi maisha magumu, unakuja unamuuliza amekujaje anakujibu amekuja kwa kuendesha gari, wakati hana uwezo wa kuona na ukiangalia Sheria ya nchi hairuhusu mtu kuendesha gari akiwa na hali hiyo ni muhimu mtu akapima macho mapema ili aweze kutibiwa'' amesema Dkt Ntomoka.