Askari ajiua kwa wivu wa mapenzi

Jumatano , 11th Jul , 2018

Askari mwenye nambari G 3777 PC Nelson William, amejiua kwa kujipiga risasi katika eneo la kambi za jeshi la Polisi alipokuwa anaishi mkoani Mara kwa kile kilichosemekana kuwa ni wivu wa mapenzi.

Kamanda wa Polisi Mkoani ya Mara Juma Ndaki.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoani ya Mara Juma Ndaki  amesema kuwa amesema askari huyo amejipiga risasi leo saa 8:30 mchana akiwa eneo la kambi za Polisi alikokuwa anaishi, kutokana na kuwa na mgogoro na aliyekuwa mpenzi wake.

Kabla ya kujipiga risasi ameacha ujumbe kuwa ameamua kujiua kutokana na wivu wa mapenzi kwa madai amekuwa hana mahusiano mazuri na mwanamke wake ambaye alikuwa ni mpenzi wake, ambaye hakuwa anaishi naye”, amesema Kamanda.

Kamanda Ndaki ameongeza kuwa  askari huyo kabla ya kuchukua uamuzi huo yaliibuka malumbano na mpenzi wake baada ya kwenda kwenye chumba cha mpenzi wake na kisha kuamua kuharibu mali alizomnunulia, baada ya kuharibiwa mali mwanamke aliamua kwenda kutoa taarifa Polisi, kitendo ambacho askari William hakikumfurahisha kwani aliona kama amedhalilishwa.

Kamanda amesema kuwa akaona njia pekee ni kuchukua uamuzi wa kujiua na ilipofika muda huo akaamua kujiua kwa kujipiga risasi, mwili wa askari huyo umehifadiwa chumba cha kuhifadhia maiti wakati taratibu za mazishi zikiendelea.