Jumanne , 13th Mar , 2018

Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), amedaiwa kusababisha kifo baada ya kumgonga mwendesha pikipiki huko eneo la Bububu, Mkoa wa Mjini Magharib Unguja. 

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Hassan Nassir Ali, amesema askari huyo, Hafidh Makame Haji (40), akiwa na gari yenye namba 5512 JWTZ O7, alimgonga Shabani Khamis (40), dereva wa pikipiki namba Z 275 FQ na kufariki dunia. 

Amesema ajali hiyo ilitokea Machi 10, mwaka huu, eneo la Bububu majira ya saa 10:15 jioni na chanzo cha ajali hakijajulikana nakuongeza kwamba jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi ili kujua chanzo cha ajali hiyo na endapo dereva huyo atabainika kufanya uzembe, atafikishwa mahakamani. 

Pamoja na hayo amewataka madereva wa vyombo vya usafiri wakiwamo madereva wa askari wa vyombo vya ulinzi na usalama, kufuata sheria za barabarani.

“Baadhi ya askari wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiwa na sare za kazini wamekuwa wakivunja sheria za barabarani wakiringia vyeo vyao, ninawaomba kutekeleza sheria za nchi,” amesema Kamanda Nasir.