Ataka Tume ya Uchaguzi iwe kama CAG

Jumanne , 14th Mei , 2019

Mwanaharakati Bob Chacha Wangwe amependekeza Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi (NEC), kupewa nguvu ya kikatiba kama aliyopewa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali CAG, ili aweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Chacha Wangwe ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye kipindi cha East Africa Breakfast cha East Africa Radio, ambapo amesema endapo akipewa nguvu hiyo itamlinda kikatiba.

"Tumependekeza kuwepo kwa mfuko maalum ambao utawafanya Tume ya Uchaguzi kujiendesha na sio mpaka kuomba Serikali kuu, pia tunapendekeza kiongozi wa Tume apewe ulinzi wa kikatiba kama ilivyokuwa kwa CAG ambaye anaweza kupambana na watu wakubwa kama Spika Ndugai." amesema Bob Chacha Wangwe.

"Kwa muundo uliopo sasa hivi, Wakurugenzi wengi walikuwa ni wagombea Ubunge ambao walishindwa, na wengine ni makada wa vyama vya siasa", ameongeza Bob Chacha Wangwe.

Hivi karibuni Bob Chacha Wangwe alifungua kesi Mahakama kuu ya Tanzania kupinga sheria inayowapa mamlaka Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia uchaguzi huku wakiwa na mahusiano na vyama vya siasa, kesi ambayo Mahakama ilimpa ushindi lakini kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jamhuri imekata rufaa.