Ijumaa , 15th Feb , 2019

Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Kangi Lugola amekemea tabia ya baadhi ya maaskari wa usalama barabarani kukamata madereva wa bodaboda kinyume na utaratibu na kusababisha malalamiko kwa bodaboda.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Kangi Lugola

Ametoa kauli hiyo leo akiwa Arusha kwenye ziara yake ya kikazi ambapo amepiga marufuku tabia ya baadhi ya maaskari waliovaa kiraia kuwakamata madereva wa bodaboda.

Kangi amesema, "ukiwa na chombo cha usafiri hata wanawake wanakupenda, lakini utakuta askari mmoja anakuja kuikamata bodaboda yako sasa utakuta mtu anapendwa na sababu ya bodaboda inasababisha mtu kukimbiwa na mwanamke."

"Nimeshaongea mara kwa mara ni marufuku kukamata bodaboda ukiwa umevaa sare za kiraia, muwakamate kwa weledi zaidi na kwa mujibu sheria", ameongeza Kangi.

Mapema wiki hii Waziri akiwa Jijini humo Arusha Kangi Lugola alizungumzia juu ya tukio la kushambuliwa kwa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu na huku akihoji ni kwanini dereva wa Mbunge huyo anayetambulikwa kwa jina la Adam Bakari, hakushambuliwa wakati walikuwa katika gari moja.