Jumatatu , 18th Feb , 2019

Baadhi ya wananchi wanaoishi katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, wameingiwa na hofu baada ya kuibuka wimbi la ubakaji wa watoto unaotekelezwa na watu wasiojulikana huku vitendo hivyo vikihusishwa na imani za kishirikina.

Picha hii haihusiani na habari

Mpaka sasa watoto wanne wamenusurika kubakwa huku wabakaji hao wakifanikiwa kumbaka mtoto mmoja ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Mapinduzi alipokuwa akitoka akitoka shuleni jioni.

Diwani wa eneo hilo, Kasmine Mwangomale amewataka watumishi wa kiroho wakiwemo wachungaji kukiweka kitongoji hicho mikononi mwa Mungu ili matukio kama hayo yaweze kukoma, huku akieleza kuwa mara nyingi maiti zinaokotwa zikiwa zimetelekezwa sehemu mbalimbali kwa muda mrefu.

Naye Mchungaji wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Vumilia Mwasenga, ameeleza kuwa Februali 17 mwaka huu walipokuwa kanisani wanaendelea na ibada, mtu mmoja alitaka kuwabaka watoto watatu wenye kati ya miaka 12 na 13.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mbeya, Debora Hokololo, amesema Jeshi la Polisi litafanya kila namna kuhakikisha wahusika wa matukio hayo wanakamatwa na kushughulikiwa na kuwataka wazazi na walezi kuimarisha ulinzi wa watoto wao kwa kuhakikisha hawawaachi peke yao majumbani ama kuwatuma peke yao kwenda madukani nyakati za usiku.

"Ina maana mnataka tuwalinde watoto wetu kama yanayotokea kule Njombe?, kule wameua na sisi tunaanza kubaka. Haya ni matunda ya kuwasikiliza waganga, naagiza kesi zote za matukio haya zifunguliwe", amesema OCD wa wilaya ya Mbeya, Debora Hokololo.