Jumatatu , 12th Apr , 2021

Imani potofu kwenye baadhi ya magonjwa ambayo yanawakabili watoto imepelekea kuvunja ndoa ya Zawadi Juma (18) baada ya kuzaa mtoto mwenye tatizo la ubongo maji, ambalo limekuwa likimsumbua tangu kuzaliwa kwake na kupelekea baba wa mtoto kumfukuza nyumbani.

Pichani Zawadi Juma akiwa na mwanae.

EATV ilifika nyumbani kwa mjomba wake na Zawadi ambapo tangu afukuzwe na mume wake ndipo mahali anapoishi naye anaelezea ugonjwa huo ulivyomuanza mtoto wake. 

"Nilijifungulia kwenye kituo cha afya Katoro tukaenda nyumbani, mtoto akamaliza wiki mbili akaanza kuugua kama vile degedege, tulilazwa hospitali akachomwa sindano tukaambiwa twende nyumbani na tuliambiwa tukiona mtoto kichwa kimeanza kukua tuwahi kumrudisha," amesema Zawadi Juma mama wa mtoto huyo.

Amesema alipoona mtoto kichwa kinaanza kukua alimwambia mumewe maelezo waliyopewa hospitalini amabapo mumewe alimjibu kuwa mtoto anakua hivyo amuache ijapokuwa kukua kwa kichwa cha mtoto huyo sio kwa kawaida.

Aidha, zawadi amewaomba Watanzania walioguswa na tatizo la mwanae waweze kumsaidia mtoto wake apone ili na yeye aweze kufanya shughuli za kumuingizia kipato, kwani mumewe amemfukuza nyumbani mpaka mtoto atakapofariki dunia ndipo warudiane.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa mkoa wa Geita, Dkt. Japhet Simeo, anasema tatizo hilo linaweza likampata mtu wa umri wowote na matibabu yanapatikana hivyo amewaomba wananchi kuacha dhana potofu juu ya magonjwa yanayotambulika hospitalini.