Ijumaa , 23rd Feb , 2018

Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe bado anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Morogoro toka jana (Alhamisi) kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko bila ya kuwa na kibali.

Hayo yameelezwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Ulrich Matei  na kudai wanaendelea na mahojiano nae ili waweze kufahamu alitoa wapi taarifa ya kufanya mkutano ya chama katika maeneo ya nje pamoja na kujua kitu alichokuwa anazungumza na wananchi wa Kata ya Kikeo iliyopo wilayani Mvomero ambapo ndipo alipokamatiwa.

"Ni kweli bado tunamshikilia Zitto Kabwe, tuna muhoji kwa sababu ya kufanya mikutano bila ya kuwa na kibali. Amekwenda kufanya mikutano ya nje maeneo ya hapa Mgeta katika Kata ya Kikeo iliyopo wilayani Mvomero", amesema Kamanda Matei.

Pamoja na hayo, Kamanda Mtei ameendelea kwa kusema "haikuwa inajulikana anazungumzia kitu gani katika mkutano wake, sasa tunajaribu kumhoji ili kuweza kufahamu mazingira yale aliendaje kule na labda alitoa taarifa sehemu gani. Mpaka sasa hivi yupo polisi na suala la dhamana lipo wazi tu anaweza kudhaminiwa muda wowote".

Mbunge Zitto Kabwe pamoja na viongozi wengine wa ACT- Wazalendo tokea  Februari 19 wapo katika ziara ya mikoa nane yenye kata zinazoongozwa na chama hicho kwa malengo ya kushiriki kazi za maendeleo na kuzungumza na kamati za maendeleo za kata hizo.