Alhamisi , 13th Jun , 2019

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amesoma makadirio ya Bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, bungeni leo Juni 13, 2019.

Waziri wa Fedha Dkt. Philip Mpango

Katika makadirio hayo Waziri mpango amesema jumla ya shilingi Tril 33.11 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika bajeti ya mwaka 2019/20.

''Mapato ya ndani ni Tril 23.05 ambayo ni 69.6% ya bajeti yote. Mapato yatakayotokana na kodi ni Tril 19.10 sawa na asilimia 12% ya pato la taifa'' - Philip Mpango.

Baadhi ya michanganuo ya bajeti 2019/2020

Tril 7.56 Mishahara,
Tril 1.44 Umeme vijijini,
Bil 788.8  Reli, Maji, Usambazaji Umeme
Bil 450 Elimu ya juu
Bil 288.5 Elimu bure,
Bil 600 Wazabuni

Katika bajeti hiyo Waziri Mpango pia amependekeza kufutwa kwa msamaha wa kodi kwenye taulo za kike.
''Kufuta kwa msamaha kodi ya ongezeko la thamani kwenye taulo za kike kwa kuwa haujawezesha kupatikana kwa bei nafuu kwa bidhaa hiyo muhimu kwa walengwa, badala yake ni kuwanufainisha wafanyabiashara'', amesema.

Aidha amependekeza kutoza ushuru wa asilimia 10 kwenye bidhaa za nywele za bandia, zinazotengenezwa ndani ya nchi na asilimia 25 zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, lengo ni kuongeza mapato ya Serikali.

Pia amependekeza kuongeza muda wa leseni ya udereva kutoka miaka 3 hadi 5, kuongeza tozo ya leseni 40000 hadi 70000, ada ya usajili wa magari 10000 hadi 50000, bajaji kutoka 10000 hadi 30000 na pikipiki kutoka 10000 hadi 20000.

Amesisitiza kuwa tozo zote zilizokuwa zinatozwa kwa dola za Kimarekani zitatozwa kwa shilingi ya Tanzania, isipokuwa kwa shehena za kemikali zinazokwenda nje ya nchi.