Balozi aeleza upendo wa Rais Kenyatta kwa WaTZ

Jumanne , 19th Mei , 2020

Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu amesema kuwa, Rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta, anao upendo wa dhati kwa Watanzania kwani siku zote hutamani Wakenya na Watanzania kuwa kitu kimoja na ndiyo maana alikuwa Rais wa kwanza kwenda Chato kumsalimia Rais Magufuli.

Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Balozi Kazungu ameyabainisha hayo leo Mei 19, 2020, wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuwaomba Watanzania kuwa na subra na kwamba ugonjwa wa Corona usiwe chanzo cha kuwagombanisha na badala yake wawaachie viongozi waweze kusuluhisha suala hilo.

"Rais Kenyatta amesema kuwa wakati wote haiangalii TZ kama jirani bali anaiangalia kama ndugu, tuwe nchi zinazoendelea na ndiyo maana alikuwa Rais wa kwanza kupanda ndege na kwenda Chato kumsalimia Rais Magufuli" amesema Balozi Kazungu.

Aidha Balozi Kazungu ameongeza kuwa, Rais Kenyatta alitamani kuja Tanzania kusherehekea na Watanzania siku ya Muungano Aprili 26, lakini uwepo wa ugonjwa wa Corona ulimfanya usije na kwamba Tanzania haijafungiwa mipaka bali kirusi cha Corona ndiyo kimepelekea yote haya.