Baraza la maaskofu lalaani Lissu kushambuliwa

Monday , 11th Sep , 2017

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limelaani shambulizi la hivi karibuni lililotekelezwa na watu wasiojulikana dhidi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu pamoja na matukio mengine ya vurugu na utekwaji.

Hayo yamebainishwa katika tamko la baraza hilo lililosainiwa na Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Beatus Kinyaiya limetolewa baada ya kikao cha kawaida cha baraza kilichofanyika kwa siku mbili Septemba 9 na 10 jijini Dar es Salaam.

“Tunapenda kutoa pole na tunasali kuwaombea wahanga wote wa vurugu hizi. Tunatamani kuona wale wote walio nyuma ya matukio haya ya vurugu, mauajji, utekwaji na utesaji wanatafutwa na kuchukuliwa hatua stahiki”

Wakizungumzia kuhusu matukio mbalimbali yaliyotokea nchini baraza hilo limesema “Katika Taifa letu sasa tunashuhudia matendo ya mauaji ya watu wasio na hatia kama ilivyokuwa kule Mkuranga, Rufiji na Kibiti, utekwaji wa watu na kuteswa, utekaji wa watoto, ulipuaji wa ofisi za watu na hivi karibuni shambulio la mbunge Lissu,”
 
Imeelezwa vurugu na mashambulizi ya aina yoyote ile yanalifedhehesha Taifa kwa kuwa matendo hayo ni dhambi, uhalifu na si utamaduni wa Mtanzania, hivyo vyombo vinavyohusika havina budi kuyakomesha mara moja.

“Tunapenda kutamka wazi na kwa nguvu zetu zote kuwa vurugu na mashanmbulizi ya aina yoyote ile yanalifedhehesha taifa, matendo haya ni dhambi, ni uhalifu na si utamaduni wetu. Tunaomba vikomeshwe mara moja” taarifa hiyo ilifafanua
 
Mbunge Tundu Lissu aliyejeruhiwa Septemba 7 kwa kupigwa risasi tano mjini Dodoma, hivi sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, jijini Nairobi nchini Kenya.