Ijumaa , 19th Apr , 2019

Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali amekubali ombi la kujiuzulu kwa Waziri Mkuu na baraza lake zima la mawaziri.

Waziri Mkuu Soumeylou Boubeye Maiga.

Soumeylou Boubeye Maiga alichukua hatua hiyo hapo jana, kufuatia wiki mbili za maandamano ya umma dhidi ya mauaji ya kiholela katika taifa hilo la magharibi mwa Afrika.

Maandamano hayo yalichochewa na mauaji ya wachungaji 160 wa jamii ya Fulani, ambayo yanashukiwa kufanywa na watu wa jamii ya Dogon, wanaoishi kwa kilimo na uwindaji. Mauaji hayo yaliitikisa nchi ya Mali, ambayo katika miezi ya karibuni imeshuhudia mauaji mengine kadhaa, yakiwemo yale ya wanajeshi 23 walioshambuliwa kwenye kituo chao.

Juzi Jumatano, bunge lilijadili uwezakano wa kura ya kutokuwa na imani na Serikali kutokana na mauaji hayo, na pia kushindwa kuwanyang’anya silaha na kuwazuwia wanamgambo wa itikadi kali.

Umoja wa Mataifa una zaidi ya wanajeshi 16,000 nchini Mali, vikiwemo vikosi kutoka Ufaransa na Ujerumani.