Jumatano , 20th Feb , 2019

Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) limelaani nguvu kubwa inayotumiwa na Jeshi la Polisi mahakamani wakati wa usikilizwaji wa kesi za viongozi wa chama hicho jambo ambalo wamemtaka Jaji Mkuu kuzisimamia mahakama zitende haki.

Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick Ole Sosopi

Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick Ole Sosopi amesema hayo leo Februari 20, 2019 licha ya Desemba, 2018 kumuandikia barua Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma bado kuna ukiukwaji wa haki mahakamani.

Sosopi, ameeleza kwamba  Februari 18, 2019 wakati wa usikilizwaji wa rufaa ya Mwenyekiti Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini,  Esther Matiko, baadhi ya wanachama walikamatwa na wengine kupigwa walipojitokeza kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo.

"Mahakama ni mhimili unaojitegemea na sehemu huru kila mtu anapaswa kwenda kusikiliza kesi kama polisi wakiendelea kuingilia mhimili huu tutegemee mahakama zetu kugeuka mahakama za kijeshi," ameeleza.

"Tulimuandikia barua Jaji Mkuu Desemba 12, 2018 kumweleza ukiukwaji wa haki unaofanywa mahakamani lakini bado vitendo hivi vimeendelea kutia doa mhimili huo, na juzi uvunjifu wa haki umefanyika nje ya ofisi yake, vijana wetu wengine walipigwa, wwengine walichukuliwa na kurudishwa muda wa mahakama ukiwa umeisha ,"  Sosopi ameongeza.

Pia baraza hilo limelaani na kusikitishwa na mauaji yanayoendelea kutokea maeneo mbalimbali nchini ikiwemo watu kufa wakiwa mikononi mwa jeshi polisi.

"Kumekuwa na mauaji yanayotokea maeneo mbalimbali Serikali imeshindwa kukomesha mauaji hayo na badala yake tunaendelea kusikia watu wanafia mikononi mwa jeshi la polisi.