Ijumaa , 18th Sep , 2020

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Kassim  Majaliwa, amesema sh. bilioni 3.7 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji katika wilaya ya Busega mkoani Simiyu.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Septemba 18, 2020 kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na wakazi wa kata za Mkula na Lamadi, wilaya ya Busega,mkoani Simiyu wakati akiwa njiani kuelekea wilayani Bunda, mkoani Mara.

Mheshimiwa Majaliwa amesema fedha hizo zimetumika kujenga mradi wa maji bomba katika kijiji cha Lukungu ambao tayari umekamilika.

Pia fedha hizo zilitumika kufanya ukarabati wa chanzo cha maji katika mradi wa maji wa Kalemela-Mkula ambao nao tayari umekamilika.

Amesema fedha hizo zimetumika kufanya upanuzi wa mradi wa maji Lamadi Kalago na Mwabayanda  ambao umefikia asilimia 50, upanuzi wa mradi wa maji Nyashimo ambao umefikia asilimia 10, ujenzi wa mradi wa maji Mkula sekondari ambao umefikia asilimia 60 pamoja na mradi wa maji Bushgwamhala ambao umefikia asilimia 100.