Bunge lapitisha muswaada sheria ya reli

Wednesday , 13th Sep , 2017

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha muswaada wa sheria ya reli ya mwaka 2017 ambayo itaondoa sheria ya reli ya mwaka 2002 ambapo kupitishwa kwa muswaada huo utaunganisha kampuni ya reli TRL na RAHCO kuwa shirika la reli Tanzania TRC

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof.Makame Mbarawa.

Awali akizungumza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof.Makame Mbarawa  amesema kuwa uamuzi wa wabunge kupitishwa muswaada huo utasaidia kupunguza changamoto za muingiliano wa kimajukumu kati ya RAHCO na TRL ikiwemo kushuka kwa mapato ambapo shirika hilo sasa litakuwa na uwezo wa kuchukua mkopo kwaajili ya uendeshaji pamoja na ujenzi wa miundombinu.

Prof. Mbarawa amesema kuwa TRC itahusika katika kushughulikia katika utoaji wa huduma za usafiri wa reli pamoja na kusimamia na kuendeleza huduma za reli ambapo wafanyakazi wote watakaohamishwa kutoka katika taasisi hizo watalipwa stahili zao kwa mujibu wa sheria.

Akiwasilisha maoni ya kambi rasmi ya upinzani kuhusu muswaada huo Mhe. Jaffar Michael imeitaka serikali kuwachukulia hatua wale wote waliosababisha hasara katika mashirika ya TRL na RAHCO pamoja na kutaka kuchukuliwa kwa tahadhari Tabora, Kigoma na Katavi kusitisha shughuli za ubomoaji kwa nyumba 3,400 pasipo fidia.