Bwege afunguka alivyotoswa na Spika

Jumatano , 11th Jul , 2018

Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF) Suleimani Bungara maarufu kama ‘Bwege’ katika kikao cha June 20, kwenye bunge la bajeti alimtaka Spika wa Bunge Job Ndugai, awe sehemu ya maandamano ya wananchi wa mikoa ya kusini ili kuishinikiza Serikali kurudisha pesa za wakulima wa zao la korosho.

Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Suleimani Bungara.

Bungara aliibua hoja hiyo, wakati wa kuchangia hoja mjadala wa mapendekezo ya Bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na kuongeza kuwa mpaka kufikia Juni 30,2018 Serikali iwe imerudisha pesa za korosho kwa wakulima takribani shilingi bilioni 81, kinyume na hapo wananchi watalazimika kufanya maandamano Julai 1, 2018.

Akizungumza kupitia KIKAANGONI ya East Africa Television inayorushwa mubashara kwenye ukurasa wake wa Facebook, Bwege amesema kuwa licha ya kutishwa kuwa wasiandamane na Spika wa bunge kuonesha kutowaunga mkono lakini wao watasubiri kikao cha bunge lijalo wataendelea kuomba kibali kwani maandamano yao ni ya amani.

Maandamano yako palepale, na nilimuomba Spika atupokelee maandamano yetu, baada ya kuonyesha kutuunga mkono. Lakini baadaye tumeona Spika kama ametuacha ila tutarudi tena kwenye vikao vyetu kujadili. Maandamano yatakuwa ya amani”, amesema Bungara.