Alhamisi , 12th Jul , 2018

Mbunge wa jimbo la Kilwa Kusini (CUF), Selemani Bungara maarufu kama 'Bwege' amedai mgogoro uliokuwepo katika chama chao umepangwa na dola kwa lengo la kukipoteza chama hicho ili kusudi kusiwepo kabisa na upinzani ambao utakuwa unachuana na chama tawala katika chaguzi mbalimba.

Mbunge wa jimbo la Kilwa Kusini (CUF), Selemani Bungara maarufu kama 'Bwege'.

Bwege amebainisha hayo wakati akizungumza kwenye kipindi cha KIKAANGONI kinachorushwa mubashara kwenye ukurasa wa facebook wa EATV kila siku ya Jumatano kuanzia saa nane mchana mpaka saa 10 alasiri baada ya kuwepo migogoro ndani ya chama chao na kupelekea kuwepo pande mbili ndani ya chama kimoja.

"Mgogoro wa CUF umetengenezwa na Dola nikimaanisha msajili wa vyama, unajua baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kumalizika kuna mchakato uliwekwa kuwa upinzani usiwepo wala ule muungano wa vyama UKAWA pia usiwepo. Ulikuwamkakati rasmi kwamba CHADEMA isiwepo na isiwe na nguvu kabisa pamoja na CUF kwa kuwa ndio vyama vilivyoonekana kuwa na nguvu katika kupambana na CCM. Kutokana na hayo kwa hiyo sisi tukapandikiziwa Prof. Ibrahim Lipumba tupambane nae ili chama chetu kiwe na migogoro kila siku ili kusudi kisiwe na nguvu", amesema Bwege.

Pamoja na hayo, Bwege ameendelea kwa kusema "kuna migogoro yenye manufaa na isiyokuwa na manufaa lakini huu wa kwetu umetengenezwa lazima uwepo ndani ya chama chetu, sisi tunapambana na ninajua tutashinda tu na tutakuwa chama kizuri chenye nguvu japokuwa nafahamu hakitakuwa na wabunge wengi lakini wataongezeka hapo baadae"

Mbali na hilo, Mbunge huyo amedai yupo tayari wamvue Ubunge ndani ya chama cha Wananchi (CUF) lakini hayupo tayari kumuunga mkono Prof. Ibrahim Lipumba kwa kuwa ni msaliti na wala haogopi kwa jambo lolote litakaloweza kumtokea.

Baadhi ya wanachama wa CUF wanaomuunga mkono Maalim Seif walianza kumuita Prof. Ibrahim Lipumba msaliti baada ya kujiuzulu madaraka yake kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na baada ya uchaguzi kuisha alirudi tena kwa mara nyingine ndani ya chama hicho huku akidai hakujiuzulu nyadhfa zake na kutaka aendelee kuwa Mwenyekiti kama awali.