Jumatano , 5th Dec , 2018

Chama Cha Mapinduzi kimewataka watumiaji wa mitandao ya Kijamii nchini kufanya hivyo katika namna ya kujenga na si kuwaundia kauli baadhi ya viongozi wake kwa lengo la kuwagombanisha na chama hicho.

Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole imedai kuwepo kwa kurasa katika mitandao ya kijamii yenye jina la Katibu Mkuu wa CCM, Dkt Bashiru Ally na kudai ukurasa huo umetoa kauli ya kumbeza Spika Mstaafu, Pius Msekwa.

Aidha chama hicho kimedai kuwa kumekuwa na taarifa potofu juu ya kufanyika kwa mkutano kati ya maafisa wa chama hicho kutoka ofisi ndogo za CCM Lumumba Jijini Dar es salaam na waandishi wa habari.

"Kumekuwapo na akaunti ya mtandao wa twiter yenye jina la Bashiru Ally na inatoa kauli ambazo sio zake kwamba amemjibu Spika Mstaafu Pius Msekwa jambo hilo ni potofu," imesema taarifa hiyo

Aidha chama hicho imezitaka mamlaka husika kuwatafuta watu ambao wamekuwa wakitumia majina ya viongozi wake vibaya na kutaka kuhimiza matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii kwa nia ya kupeana habari bila kuathiri usalama.

Hivi karibuni kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini Pius Msekwa alitoa kauli iliyoashiria kumkosoa Katibu Mkuu CCM, juu ya njia aliyoitumia kumuita kada wake Bernard Membe ili ajibu tuhuma zinazomkabili.