Jumatano , 15th Aug , 2018

Baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Rukwa kumfukuza diwani hivi karibuni na mwingine kujiuzulu leo, Mwenyekiti wa chama hicho mkoa huo Shadrack Malila maarufu Ikuwo amesema wengi wanaohama ni wasaliti wanarudi kwao.

Picha ya uzinduzi wa moja ya mashina ya CHADEMA na haihusiani na habari.

Akiongea na www.eatv.tv muda mfupi baada ya diwani wa Kata ya Mambwenkoswe wilayani Kalambo Kanowalia Siwale kutangaza kujiuzulu na kuhamia CCM, Malila amesema alijua hilo tangu mapema kwasababu amekuwa akimweleza mambo mengi ikiwemo kupata vitisho kutoka kwa viongozi wa juu wilaya.

''Wanaohama sio wanachama halisi wa CHADEMA na hawajui dhumuni la chama hiki kwahiyo wanapoteteleshwa na vitisho au hongo huwa wanaamua kusaliti na wengi wao huja na vijisababu vyepesi kama vitisho lakini mwisho wa siku ukifuatilia unagundua wanarudi walikotoka na huwa tunawabaini mapema ndio maana wengine tunawatimua'' amesema.

Aidha Malila ameongeza kuwa kuondoka kwa wanachama hao ambao ni wasaliti kunakiongezea uimara chama hicho kutokana na kubaki na wanachama ambao ni waaminifu na wanajua dhumuni na thamani ya chama hicho. Pia ameweka wazi kuwa wanaendelea na uchunguzi kwa baadhi ya madiwani wanaodaiwa kukisaliti chama na wakibaini hilo watatoa adhabu sitahiki.

Amemaliza kwa kusema kuwa kinachowafanya waamini kuwa viongozi wanaohama ni mamluki ni kitendo cha CCM kuwapa dhamana ya kugombea tena katika maeneo waliyotoka. Jumapili Agosti 12, CHADEMA mkoa wa Rukwa ilitangaza kumfuta uanachama diwani wa kata ya Majengo wilaya Sumbawanga Bw. Dickson Mwanandenje.