Ijumaa , 14th Sep , 2018

Chama cha Mapinduzi (CCM), kimesema uchaguzi mdogo wa marudio unaotarajiwa kufanyika Septemba 16, 2018 umekuwa uchaguzi wenye mtihani kwao, kwa madai kukiukwa kwa baadhi ya sheria za uchaguzi ya mwaka 1985 kutoka wapinzani wao wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Katibu wa Itikadi wa Uenezi Humphrey Polepole

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Katibu wa Itikadi wa Uenezi Humphrey Polepole amesema wapinzani wao wamekuwa wakitumia lugha zisizo na staha pamoja na utoaji wa rushwa kwenye mikutano ya kampeni unaofanywa na baadhi ya viongozi wake.

Polepole amesema "wenzetu hawakutaka kuheshimu sheria za vyama vingi, hawakufata maadili ya uchaguzi wenzetu wameyapuuza yote.., kinyume na sheria ya uchaguzi ya mwaka 1985, niwaambie tu TAKUKURU, chama cha CHADEMA wanagawa fedha na sukari kule Monduli na tunalifahamu hilo, tunaomba lifuatiliwe".

Polepole akaongeza, "Kamati ya maadili ya uchaguzi ya jimbo la Ukonga ilitoa adhabu kwa viongozi wa CHADEMA waliotumia lugha chafu kwenye kampeni ikiwemo kumtukania utu wake Mwita Waitara, ikiwataka waombe radhi hadharani lakini wamekaidi mpaka sasa".

Katika hatua nyingine Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi wa CCM amesema licha ya changamoto hizo wana uhakika kuwa chama chao kitashinda chaguzi hizo.

Uchaguzi wa majimbo ya Monduli  na Ukonga unarudiwa kutokana waliokuwa wabunge wake kwa tiketi ya CHADEMA, Julius Kalanga kwa upande wa Monduli na Mwita Waitara kwa upande wa Ukonga kujiuzulu huku wakiwania tena nafasi hiyo kupitia CCM.

Katika chaguzi hizo Tume ya Uchaguzi ilitangaza marudio ya uchaguzi katika kata 20 pamoja na majimbo matatu ikiwemo jimbo la Korogwe vijijini ambalo mgombea wake Timotheo Mzava wa CCM alipita bila kupingwa na pia katika kata chaguzi za kata 20 chama hicho kilipita bila kupingwa kwa kata 12.