Alhamisi , 16th Aug , 2018

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya jamii zikidai kuwa kamati kuu ya chama hicho imempitisha kuwania nafasi ya Ubunge jimbo la Monduli Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa.

Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa.

Kamati Kuu ya (CHADEMA), imekutana katika kikao chake maalum jana Jumatano Agosti 15, 2018 kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali kuhusu chama hicho na taifa kwa ujumla.

Akizungumza na tovuti ya www.eatv.tv Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arusha, Amani Golugwa amesema kuwa taarifa za kuteuliwa Lowassa hazina ukweli wowote kwani kufanya hivyo ni kumshusha hadhi Waziri Mkuu huyo mstaafu na kudai kuwa hadhi yake kwa sasa ni nafasi ya urais.

Hayo sio mapendekezo ya kamati kama wanavyosema na hizo ni taarifa za uzushi na zinafanywa na wapinzani wetu kutaka kutuchafua, hakuna mgombea aliyepitishwa na mapendekezo yote yaliyotolewa ni ya awali,” amesema Golugwa.

Akizungumzia uamuzi wa Fred Lowassa kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha wanaowania kuteuliwa na chama hicho kugombea ubunge jimbo la Monduli, Golugwa amesema baada ya kushauriana, vikao vya uteuzi vilikubali kuondoa jina lake.

Fred ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, alichukua fomu ya kuwania ubunge jimbo hilo wiki iliyopita lakini jana aliomba kujiondoa kwakile alichodai kuwa bado muda wake muafaka licha ya kuonekana kuungwa mkono na wanachama wengi awali.

Baada ya kujiondoa, Chadema kimempitisha diwani wa kata ya Lepurko, Yonas Masiaya Laizer kuwania ubunge wa jimbo hilo, kufuatia aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Julius Kalanga, kuachana na Chadema na kuachia ubunge na kuhamia CCM, ambapo Kalanga ameshateuliwa na CCM kugombea tena jimbo hilo.