Jumatatu , 1st Apr , 2019

Uongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, umesema kuwa msimamo wao ni ule ule kwamba hautashiriki uchaguzi kwenye jimbo la aliyekuwa Mbunge wake Joshua Nassari, kutokana na sababu zao za awali kuwa hakuna uwanja sawa wa ushindani.

Joshua Nassari

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt Vincent Mashinji ambaye maamuzi ya kikao chao kilichofanyika hivi karibuni Jijini Dar es salaam kikiongozwa na Mwenyekiti wake Freeman Mbowe wameazimia kutoshiriki uchaguzi huo.

"Hatujabadili msimamo wa chama kutoshiriki chaguzi hizi, kwa sasa mtazamo wetu ni Uchaguzi Mkuu, na chama ndicho kinachoamua, kuhusu Nassari mwenyewe kama alikuwa ndani ya chama kwa ajili ya madaraka anaweza kuondoka”, amesema Dkt. Vicent Maashinji.

www.eatv.tv imejaribu kumtafuta Joshua Nassari ili kuzungumzia hatma ya Ubunge wake ikiwa siku chache baada ya Mahakama kuu Kanda ya Dodoma kutoa uamuzi wa kutobadilisha uamuzi, lakini simu yake haikupatikana.

Machi 14, 2019 Spika wa Bunge Job Ndugai, alitangaza kumvua Nassari ubunge wa jimbo la Arumeru Mashariki kwa makosa ya mahudhurio hafifu bungeni ikiwemo kukosa vikao vya mikutano mitatu ya bunge.