Chama cha Wafanyakazi chamjia juu Makonda

Jumanne , 13th Feb , 2018

Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) kimelaani kitendo kikichofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda cha kuwavua madaraka hadharani watumishi na kusema ni kitendo cha kinyama alichofanya. 

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU), Rashid Mtima amesema hayo leo Februari 13, 2018 wakati akiongea na waandishi wa habari na kusema kitendo kilichofanywa na Mkuu wa Mkoa si cha kiuungwana.

"Tunacholani ni kitendo cha Mkuu wa Mkoa akiwa kwenye mkutano wa hadhara kuhukumu watendaji wa Serikali za Mitaa hiyo haipo kisheria na tunaomba na kuwataka wanasiasa wafuate utaratibu katika kusimamia nidhamu ya watumishi. Sisi tunatambua na kusema kama chama kitendo alichofanya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam si tu cha kinyama lakini kimewadhalilisha watumishi wetu kwenye Serikali za Mitaa na imeonyesha kutoheshimiwa kwa utawala bora wa kisheria kinyume na haki za binadamu" alisisitiza 

"Wapo watumishi Februari 10, 2018 Mkuu wa Mkoa alitangaza kuwavua madaraka, wewe umetamka neno ambalo mtu limemuingia kwa kumuumiza anapoteza fahamu halafu unainuka unasema Dar es Salaam hoyeee, tafsiri yake ni nini sisi kama viongozi, nilitarajia lile jambo watu tulipokee kwa masikitiko" alisema Mtima