Alhamisi , 19th Mar , 2020

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa kinaangalia namna ambayo itawawezesha kuwasafirisha Wabunge Ester Bulaya, Halima Mdee na Jesca Kishoa kwa ajili ya kupatiwa matibabu nje ya nchi kwa kuwa hali zao bado hazijatengemaa.

Wabunge Ester Bulaya, Halima Mdee na Jesca Kishoa wakiwa hospitalini.

Akizungumza leo Machi 19, 2020, na EATV&EA Radio Digital, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema amesema kuwa kulingana na hali ya maambukizi ya Virusi vya Corona ilivyo kwa sasa inawawia vigumu kuchukua maamuzi yoyote, kwakuwa nchi walizodhamiria kuwapeleka tayari zimekwishakumbwa na visa vya ugonjwa huo.

"Kina Ester wameruhusiwa juzi, isingekuwa Corona tulikuwa tunafikiria kuwapeleka nje kupata matibabu zaidi, lakini bado tunawaza nini cha kufanya, hali zao bado hazijatengemaa, hasa Ester aliyeumia ndani huwezi jua nini haswa kinasumbua, tulitaka kuwapeleka kwenye nchi ambazo zina matibabu mazuri kuliko sisi kama Kenya na Afrika Kusini" amesema Mrema.