CUF waituhumu CCM na Ofisi ya Msajili

Ijumaa , 15th Mar , 2019

Naibu Mkurugenzi wa Habari wa CUF inayounga mkono upande wa Maalim Seif, Mbarala Maharagande ameituhumu ofisi ya msajili wa Vyama vya Kisiasa, pamoja na Chama cha Mapinduzi CCM kwamba wao ndio wanaoihujumu CUF kwa kupanga kubadilisha Katiba.

Mbarala ameyasema hayo huku akiainisha kwamba huo ni ukweli uliowazi kwamba Lipumba akishirikiana na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza na CCM wamekaa kupanga mabadiliko ya Katiba ya chama.

Mbarala amesisitiza kwamba Katiba ya Chama cha Wananchi, CUF haiwezi kurekebishwa kwa maoni, ushauri kutoka kwa CCM.

"Mabadiliko ya Katiba ni mchakato. Lipumba na genge lake wamejifungia na Msajili Mutungi, Sisty Nyahoza na CCM kupanga Mabadiliko. CUF chini ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad kamwe haitakuwa wakala wa CCM kuhujumu vyama vya siasa vingine na kuwasaliti Watanzania".

Pamoja na hayo, Mbarala amesema kwamba mambo yote hayo yanayofanywa na Lipumba yatapingwa kisheria Mahakamani.