Jumapili , 31st Mei , 2020

Taasisi  ya kuzuia na kupambana na rushwa Takukuru Mkoani Mbeya imethibisha kumkamata  Diwani wa Viti Maalum wilaya ya Kyela, Tumain Mwakatika kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa kinyume na sheria ya Takukuru namba 11 ya mwaka 2007.

Makao makuu ya kupambana na rushwa Takukuru Mbeya

Akithibisha hilo Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mbeya, Julieth Matechi amesema  Diwani huyo amekamatwa  na maofisa wa Taasisi hiyo katika Wilaya ya Kyela  Mei 30 mwaka huu wakati akigawa fedha kwa wajumbe wa jumuiya ya umoja wa wanawake Tanzania "UWT" ambao walikuwa wakishiriki Ibada ya maziko ya aliyekuwa Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, wilaya ya Rungwe Esther Mwakipesile.

Matechi amesema uchunguzi wa Takukuru wilaya ya Kyela ulibaini kuwa diwani huyo alikuwa akigawa fedha kwa wajumbe  ambao walihudhuria ibada ya maziko ya Mwakipesile.

Aidha amesema maofisa ambao walijipanga vyema kufuatilia vitendo hivyo vya rushwa kuelekea uchaguzi mkuu na walimuweka chini ya ulinzi na kumshikilia kisha kumchukua kwa ajili ya mahojiano ambayo yalifanyika kwenye ofisi za Takukuru Kyela.