Jumatatu , 26th Jul , 2021

Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ametoa onyo kali kwa watumishi wa umma wanaofanya vitendo vya wizi wa mali na vifaa vya umma na kusema kuwa kwa yeyote atakayebainika kuhusika na wizi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake

Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango (watatu kushoto) akiweka
jiwe la msingi Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini iliopo Manispaa ya Mikindani mkoani Mtwara, Julai 26,2021.

Dkt Mpango ametoa onyo hilo leo, wakati akiweka jiwe la msingi la Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini Mtwara, lililojengwa na NHC kama Mkandarasi, na kusema kuwa hatokuwa mpole wala kuchekea wizi wa mali na vifaa vya umma.

“Natanguliza onyo kali kwa watumishi wasiowaaaminifu katika sekta ya afya na hasa upande wa manunuzi kwenye bohari yetu ya dawa, idara za tehema, maduka ya dawa niwaambie serikali ya awamu ya sita itachukua hatua kali sana kwa yeyote atakayefanya uzembe au kuhusika na wizi dawa,” amesema Dkt. Mpango.

 “Mtumishi yeyote tutayembaini amehusika na wizi wa dawa na vifaa vyake, Mhe Naibu Waziri wa Afya kamwambie Katibu mkuu wako, cha kwanza muondeeni kazini tumechoka na msiishie hapo vyombo vya sheria vipo apelekewe Mahakamani, niwaambie kabisa tutataifisha chochote alichonacho ili kufidia upotevu wa dawa zetu,” ameongeza Dkt. Mpango.

Samabamba na hilo Dkt. Mpango ameendelea kuwasihi wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya janga la corona kwani wimbi la sasa linauwa haraka zaidi.

“Ugonjwa wa corona upo, tulifanya vizuri sana tulipopigwa na wimbi la kwanza na la pili baada ya hapo tukaona Mungu ameshalifukuzilia mbali tukajisahau, limekuja wimbi la tatu baya zaidi hata dalili zake zinatofautiana, linaua haraka zaidi,” amesema Makamu wa Rais Dkt. Mpango.