Alhamisi , 13th Aug , 2020

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), imesema kuwa imefanya uchambuzi wa Tetemeko la Ardhi lililotokea usiku wa kuamkia leo Agosti 13, 2020 na kubaini kuwa Tetemeko hilo halikuwa na nguvu kubwa na hakuna maporomoko ya ardhi yaliyojitokeza baharini ambayo yangeweza kuzalisha Tsunami.

Tetemeko.

Imeelezwa kuwa Tetemeko hilo la Ardhi lilikuwa na ukubwa wa kipimo cha 5.9 katika eneo la Kusini Mashariki mwa Mkoa wa Pwani katika Bahari ya Hindi, ambalo lilitokea katika eneo la chini ya Bahari.

TMA imesema kuwa itaendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa baharini na kutoa taarifa endapo kutajitokeza mwendelezo wa matetemeko katika eneo la Bahari, na  kuongeza kuwa hakuna athari zilizojitokeza au zinazotarajiwa katika mifumo ya hali ya hewa ya Bahari kutokana na tetemeko hilo.

Mbali na hayo TMA pia imetoa ushauri kwa watumiaji wa eneo la Bahari kutokuwa na hofu na kuendelea na shughuli kwa kuzingatia taarifa ya hali ya hewa Baharini kama ilivyotolewa awali na Mamlaka.

Baadhi ya maeneo ambayo yalikumbwa na Tetemeko hilo kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni pamoja na Tabata, Mikocheni, Posta, Buza, Ubungo na Kimara.