Alhamisi , 13th Jun , 2019

Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imeweka mfumo maalum wa udhibiti wa usalama wa chakula kinachozalishwa ndani ya nchi  na kile kinachoingizwa kutoka nje ili kuwahakikishia afya bora kwa walaji.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa TFDA, Adam Fimbo.

Mfumo huo ni kufanya tathmini ya vyakula vilivyofungashwa, kusajili maeneo na kutoa vibali vya biashara za vyakula, kufanya ukaguzi wa vyakula katika soko pamoja na ukaguzi wa maeneo ya kusindikia, kuhifadhia na kuuzia vyakula.

Akizungumza wakati akifungua Semina ya siku mbili kwa waandishi wa Habari iliyofanyika Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA Adam Fimbo, alisema mfumo huo pia unalenga kuchunguza sampuli za vyakula katika maabara.

“Mfumo huu unahakikisha kila mtanzania anatumia chakula salama, na tunaanzia mipakani na kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini” alisema Fimbo.

Baraza Kuu la umoja wa mataifa kupitia kikao chake cha Desemba 28, 2018, ilipitisha siku ya usalama wa Chakula Duniani kuwa   Juni 7 ya kila mwaka ambapo kwa mara ya kwanza Duniani kote siku hiyo ilianza mwaka huu wa 2019.

Kwa mujibu wa shirika la Afya Duniani WHO takribani Watu Milioni 600 Duniani sawa na Mtu mmoja kati ya watu 10 huugua kila mwaka kutokana na kula chakula kisicho salama na kati yao watu 420,000 hufariki  na huku watoto wakiwa  125,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano ambapo kwa Bara la Afrika zaidi ya watu milioni 91 wanakadiriwa kuugua huku watu 137,000 hufariki dunia kila mwaka.