Jumatatu , 15th Oct , 2018

Familia ya mfanyabiashara maarufu nchini Mohammed Dewji imetangaza dau la shilingi bilioni moja kwa yeyote atakayefanikisha kupatikana kwa mfanyabiashara huyo aliyetekwa Alfajiri ya Oktoba 11.

Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari, msemaji wa familia hiyo Azim Dewji amesema kuwa kwa atayefanikisha kupatikana kwa mfanyabishara huyo awasiliane na familia hiyo.

"Katika kuhakikisha kuwa mtoto wetu mpendwa anapatikana mapema familia inapenda kutangaza zawadi nono ya shilingi bilioni moja za kitanzania, na atakayesaidia kutoa taarifa hizo zitabaki siri baina yetu"

Taarifa za kutekwa kwa mfanyabiashara huyo anayekadiriwa kuwa na utajiri wa Sh3.5 trilioni zilianza kusambaa Alhamisi saa 1:00 asubuhi katika mitandao ya kijamii, kabla ya polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam kuthibitisha saa mbili asubuhi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam Lazaro Mambosasa amesema kuwa mpaka sasa watu 26 wanashikiliwa ili kusaidia jeshi hilo katika uchunguzi.