Jumatatu , 5th Aug , 2019

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara RPC Juma Ndaki,  amesema hali ya gari la Mkuu wa Mkoa huo Adam Malima, hairidhishi kabisa hii ni baada ya gari hilo kugongeshwa na mtoto wa dereva na kuharibika vibaya.

Gari hilo baada ya kupata ajali

Gari hilo lenye namba STL 5962 liligongeshwa jana Agosti 4, 2019, maeneo ya Kwangwa Musoma mjini na mtoto anayedhaniwa kuwa ni wa dereva wa Mkuu wa Mkoa, baada ya kulichukua bila ridhaa ya baba yake na kuondoka nalo.

''Gari hiyo aliiacha kwenye silencer ili akitoka mgeni airudishe kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa, lakini wakati anaongea na mgeni yule mtoto akaingia ndani ya gari nakuondoka nayo, sasa katika uendeshaji ikamshinda ikawa imetoka nje ya barabara na kugonga daraja,  ikawa imehabribika kwa kiasi kikubwa, na mtoto kakimbizwa hospitali kutokana na majeraha aliyoyapata'' amesema RPC Ndaki.

Kufuatia ajali hiyo kijana huyo amelazwa hospitali kutokana na kuumia sehemu ya kifua na mkono, ambapo baada ya dereva ( Baba yake) kukuta hali ya gari si nzuri na yeye alipata mshituko na kuanguka na kupelekwa hospitali.

Aidha Kamanda Ndaki amesema kuwa Jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi, na kwamba watawachukulia hatua stahiki wote waliosababisha ajali hiyo akiwemo dereva aliyeacha gari na kisha kuchukuliwa kizembe.