Jumamosi , 23rd Jun , 2018

Baada ya serikali kutangaza ujenzi wa vyumba vya madarasa 478 kwa nchi nzima ili kuwapatia nafasi zaidi ya wanafunzi elfu 21 waliokosa nafasi ya kujiunga kidato cha tano mwaka 2018 kutokana na ukosefu wa madarasa ya kutosha, taasisi ya Hakielimu imepongeza serikali kwa hatua hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa hakielimu Dkt. John Kalage

Akizungumza leo na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam, kuhusiana na suala hilo Mkurugenzi Mtendaji wa hakielimu Dkt. John Kalage amesema kiasi cha fedha shilingi Bilioni 29 kilichotengwa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hasa ya madarasa na mabweni nchini zitumike ipasavyo katika kutekeleza mradi huo.

"Kufanikisha ujenzi wa madarasa 478 na mabweni 269 kwa ubora ndani ya miezi miwili ni ngumu kwa kweli, hasa ikizingatiwa hatua za awali za kuandaa ardhi, wataalam na mambo mengine zilikuwa hazijafanywa,"amesema Kalage.

Aidha Dkt. Kalage ameongeza kuwahii ni hatua kubwa kwa serikali kudhamiria kupunguza kero ya ukosefu wa vyumba vya madarasa, lakini pia ameikumbusha serikali kupitia wizara ya elimu sayansi na teknolojia juu ya changamoto ya uhaba wa waalimu na vitendea kazi shuleni.

Hivi karibuni, Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa TAMISEMI Mheshimiwa Suleiman Jafo alitangaza kuwa zaidi ya Bilioni 29 zimetolewa na serikali kutumika kujenga vyumba vya madarasa 478 na mabweni 269 katika kipindi cha miezi miwili tuu.