Jumatatu , 19th Mar , 2018

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, James Karayemaha, ameagiza Tito Machibya maarufu kama Nabii Tito, kufikishwa mahakamani ili kuendelea na kesi yake au apate maelezo kamili ya kwa nini mtuhumiwa huyo hafikishwi mahakamani.

Hakimu Karayemaha ametoa maagizo hayo leo baada ya kuelezwa kuwa Nabii Tito hakufikishwa mahakamani kutokana na kuwa bado anaendelea kupatiwa matibabu ya ugonjwa wa akili unaomkabili kwenye kituo cha magonjwa ya akili katika hospitali ya Mirembe.

Hakimu Karayemaha hakuridhika na majibu hayo na kuagiza Nabii Tito kufikishwa mahakamani hapo kuendelea na kesi yake au kama kuna ulazima wa kutokufika mahakamani basi apelekewe maelezo rasmi yanayomkwamisha mtuhumiwa huyo kufika mahakamani.

Hata hivyo askari magereza aliyewaleta mahabusu Mahakamani amedai kwamba, tangu mahakama ilipoamuru Nabii Tito afanyiwe vipimo vya kujua kama ana ugonjwa wa akili mwezi Februari mwaka huu bado mtuhumiwa huyo hajamaliza siku za uchunguzi wa vipimo hivyo, na kwamba, bado yupo Hospitali ya Mirembe na hayupo mahabusu kwenye gereza la Isanga.

Kesi ya Nabii Tito imeahirishwa hadi April 5 mwaka huu itakapotajwa tena.