Alhamisi , 6th Dec , 2018

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeridhia mbunge wa Jimbo la Kawe (CHADEMA), Halima Mdee kuendelea na majukumu yake ya ubunge nje ya nchi yaliyomfanya ashindwe kufika mahakamani leo Desemba 6, 2018 kwa ajili ya kesi ya jinai inayomkabili.

Mbunge wa Jimbo la Kawe (CHADEMA), Halima Mdee.

Mdee na viongozi wakuu wa CHADEMA, akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe walikabiliwa na mashtaka 13 ya uchochezi, uasi na kuhamasisha wafuasi wao kutenda makosa, hakuweza kufika mahakamani wakati kesi yao ilipotajwa leo.

Akitoa uamuzi, Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri amesema kuwa alipokea nakala ya barua ya Bunge ikimwombea ruhusa Mdee na kwamba amekubali aendelee na shughuli zake hizo.

Kuhusu Heche amesema pia anamruhusu aendelee na ruhusa yake ya kumuuguza mkewe ambayo alishampatia, hata hivyo amewataka wote wawepo tarehe nyingine kesi hiyo itakapotajwa. Ameiahirisha kesi hiyo hadi Desemba 21, 2018.

Mbali na Mdee Mdee, Heche na Mbowe, washtakiwa wengine ni katibu mkuu, Dkt. Vicent Mashinji; naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar) na mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa,  Esther Matiko na mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama,  kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.