Alhamisi , 26th Mar , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amesema kuwa vikao vya kawaida vya watendaji wa Serikali vitaendelea na hata Uchaguzi Mkuu utafanyika kama ilivyopangwa.

Rais Magufuli

Amesema hayo leo, Machi 26, 2020 katika hafla ya kupokea ripoti kutoka Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali CAG na ripoti ya TAKUKURU katika Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma.

Rais Magufuli amesema kuwa hata nchi ambazo zimeathirika zaidi na virusi vya Corona, bado mabunge na mabaraza yao yanaendelea na kusema kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utafanyika.

"Hatujazuiliwa kukutana, leo nimesoma gazeti moja linasema 'Madiwani wafanya kikao cha Madiwani', sijui alifikiri vikao vya madiwani vimezuiliwa kwa sababu ya Corona?. Sisi tunaendelea kukutana katika mikutano hii ya kawaida na hata Bunge ndio maana linaendelea", amesema Rais Magufuli.

"Kazi lazima iendeleea kufanyika na uchaguzi tutafanya tu, wapo wengine wanafikiri nitaahirisha, ni nani anataka kukaa kwenye maofisi haya muda wote huu", ameongeza Rais Magufuli.

Katika ripoti ya ukaguzi iliyowasilishwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG, Charles Kichere, jumla ya hati 1084 za Taasisi za Serikali Kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma, miradi ya maendeleo na Vyama vya Siasa kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2019 zimekaguliwa. Hati zinazoridhisha ni 1017, zenye shaka ni 46, hati zisizoridhisha ni 7 na hati mbaya 12. 

Pia Rais Magufuli amempandisha cheo aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali, John Mbungo kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo kwa kazi nzuri aliyoifanya ikiwemo ya kurejesha bilioni 8.8 walizodhulumiwa wananchi.