Jumapili , 15th Jul , 2018

Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu amewataka wanachama na viongozi wa chama hicho kutumia vizuri fursa ya uchaguzi mdogo wa marudio uliopangwa kufanyika Agosti 12 mwaka huu kwa kupambana kiakili ili waweze kushinda chaguzi hiyo.

Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu

Lissu ametoa kauli hiyo leo Julai 15, 2018 kupitia ukurasa wake maalum wa kijamii na kusema uchaguzi huo wa marudio katika Jimbo la Buyungu Mkoani Kigoma na kata 77 Tanzania Bara ni fursa kwao kuendelea kupigania haki za wananchi na utawala bora.

"Hakuna uchaguzi mdogo, kila uchaguzi ni muhimu katika mazingira halisi ya sasa ya kisiasa. Uchaguzi wa marudio wowote ule una kuwa na ugumu wa kipekee, tutafanyiwa na tayari tunafanyiwa kila aina ya fujo na CCM na mawakala wake kwenye Tume ya Uchaguzi na vyombo vya dola", amesema Lissu.

Pamoja na hayo, Lissu ameendelea kwa kusema "wajibu wetu ni kupambana kwa akili na maarifa ya hali ya juu ili kuzishinda fujo hizo na kushinda chaguzi hizo. Najua ni kazi ngumu, haijawahi kuwa rahisi mahali popote. Hatuna mjomba au shangazi wa kutufanyia kazi hii, au wa kumlilia baadaye tusipoifanya vizuri. Ni jukumu letu pekee".

Kauli hiyo ya Tundu Lissu imekuja yakiwa yamepita masaa machache tangu dirisha la kuanza kupiga kampeni kufunguliwa kwa kuomba ridhaa ya wananchi katika maeneo ambayo yatakuwa yana uchaguzi nchini Tanzania ifikapo Agosti 12 mwaka 2018.