Hii ndiyo idadi ya wagonjwa wa Corona Tanzania

Jumatatu , 1st Jun , 2020

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kuwa, idadi ya wagonjwa wa Corona hapa nchini imepungua kwa kiasi kikubwa na kubaki na wagonjwa wanne pekee walio katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy ameyabainisha hayo leo Juni Mosi, 2020, wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ya uzinduzi wa jengo la Bodi ya Mkonge lililopewa jina la Mkonge House, na kusisitiza kuwa kwa takwimu hizi watu wasijisahau, bali waendelee kujikinga na ugonjwa huo.

"Hapa Tanga hatuna mgonjwa wa Corona, DSM katika Hospitali ya Amana wamebaki 3, Mloganzila 1, Kibaha hatuna mgonjwa, Mwanza hatuna mgonjwa jambo la kusisitiza ni kuwa Corona bado ipo tuendelee kujikinga, na mimi nilisema pale Ikulu Dodoma katika Uwaziri wangu sikuwahi kupitia kipindi kigumu kama hiki cha Corona kwakweli nilihenya" amesema Waziri Ummy.