Jumapili , 14th Oct , 2018

Vuguvugu la wabunge wa vyama vya upinzani kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuunga mkono jitihada za Rais, Dkt John Pombe Magufuli bado linaendelea ambapo mpaka sasa jumla ya wabunge nane wameshakumbwa na vuguvugu hilo.

Saed Kubenea

Www.eatv.tv imefuatilia baadhi ya matamko na maandiko ya Mbunge wa jimbo la Ubungo, Saed Kubenea juu ya nguvu kubwa anayoitumia kukanusha madai ya kuwa huenda akatangaza kukihama chama chake cha CHADEMA muda wowote, hali ambayo ni tofauti kwa baadhi ya wabunge wengine wanaotajwa.

Hivi karibuni kupitia baadhi ya vyombo vya habari ilitajwa orodha ya majina ya wabunge 15 wenye hatihati ya kuhama vyama vyao akiwemo, Mbunge Ester Bulaya, John Mnyika, aliyekuwa Mbunge wa Ukerewe Joseph Mkundi ambaye nae amehama CCM na Saed Kubenea ambaye yeye ameonekana kuzua sintofahamu mpaka sasa kutokana na nguvu anayoitumia kujibu madai hayo.

Disemba 2017, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Kubenea alikanusha taarifa za kutaka kuhamia CCM kwa kile alichokieleza jambo hilo linaenezwa na baadhi ya wabaya walio ndani ya chama chake.

Disemba 2017, Kubenea alitembelea moja ya chombo cha habari cha televisheni nchini kukanusha taarifa ya kukihama chama chake.

Oktoba 2018, Kubenea aliandika waraka aliousambaza kwenye mitandao ya kijamii akimkosoa moja ya mwandishi kuwa alimnukuu vibaya kwenye habari aliyoiandika.

Oktoba 2018, Mbunge huyo aliandika waraka mwingine akilikosoa moja ya gazeti nchini lililomtaja kwenye orodha ya wabunge 15 ambao watakihama chama hicho muda wowote.

Oktoba 2018, kilisambaa kipande cha sauti iliyosadikika kuwa ni sauti ya Mbunge huyo pamoja na Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu iliyosikika wabunge hao wakidai kutoridhishwa na baadhi ya mambo ndani ya chama chao cha CHADEMA.

Katika kipindi cha mwaka mmoja mbunge huyo ameonekana kutoa matamko zaidi ya matano kukanusha taarifa hizo huku madai yake makubwa akidai taaria hizo zinaendeshwa na baadhi ya makada wenzake wa CHADEMA hali maswali mbalimbali ikiwemo.

Je ni kweli atahamia CCM kabla ya mwaka haujaisha?, kwanini tuhuma za yeye kuhama chama kwake ziwe na nguvu kubwa sana kuliko wabunge wengine?.

Kwanini Mbunge huyo anatumia nguvu kubwa kukanusha taarifa za kuhamia CCM tofauti na wabunge wengine wanaotajwa?.

Kama anavyodai kuwa anadai taarifa hizo zinaenenzwa na baadhi ya makada wa chama chake, je haaminiki ndani ya chama hicho au chama kina malengo mabaya dhidi mbunge huyo. Je ndie mbunge aliyetajwa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara kuwa atahamia CCM?.

Hivi karibuni moja ya waraka wake Kubenea alisema “narejea tena na tena, kwamba sina mpango wa kuondoka CHADEMA, sijawahi kuzungumza na mtu yoyote yule wa CCM kuwa nataka kujiunga na chama chao, hii ni kwasababu, mpaka sasa, mimi binafsi, sijaona sababu zinazojitosheleza kunishawishi kuondoka CHADEMA na kujiunga na chama kingine.”