Jumapili , 6th Oct , 2019

Mahakama ya Wilaya ya Lindi, mkoani Mtwara, imemuhukumu mkazi wa Mitema aliyefahamika kwa jina la Kijazi Ally (29), kifungo cha miezi 36 jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa mawili, likiwemo la kuvunja nyumba usiku na kuiba.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mshtakiwa aliulizwa kama anazo sababu za msingi, zitakazoishawishi Mahakama isimpe adhabu kali kwa makosa aliyokutwa nayo, ambapo katika kujitetea kwake alikiri kosa hilo na kudai kuwa ilikuwa ni mara yake ya kwanza na alilitenda kwa sababu ya njaa na kuahidi kutorudia tena.

Baada ya utetezi huo, Hakimu Kiswaga alimuuliza Mwanasheria wa Serikali Godfrey Mramba, kama ana kumbukumbu ya makosa ya zamani kwa mshtakiwa,ambapo alijibu kuwa hana lakini aliomba apewe adhabu kali, kwani ni mwizi mzoefu anayesumbua wakazi wa Mji wa Lindi.

Mramba alisema licha ya kutokuwa na kumbukumbu kwa makosa ya zamani kwa mshtakiwa,lakini tayari anakabiliwa na kesi nyingine inayohusu vitendo vya uvunjaji wa nyumba za watu nyakati za usiku na ipo katika Mahakama hiyo.

Kufuatia kesi  hiyo namba 14/2019, Hakimu Kiswaga alimhukumu mshtakiwa huyo kifungo cha miezi 36.