Jumatano , 19th Jun , 2019

Kufuatia uwepo wa taarifa za  tishio la shambulio katika maeneo ya Masaki, hususani katika hoteli na migahawa, Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa amesema wanazo taarifa hizo na wanafuatilia.

Kamanda Lazaro Mambosasa

Akiongea na www.eatv.tv Kamanda Mambosasa, amesema taarifa hizo zipo, na wao kama jeshi la Polisi wanaendelea kufuatilia kwa karibu.

''Ni kweli taarifa zipo zinasambaa na sisi tunafuatilia, watu watulie tu kwasababu unaweza ukakuta mtu mmoja tu ameanzisha'', Mambosasa.

Aidha kabla ya kuongea na Mambosasa, www.eatv.tv ilimtafuta Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi Kinondoni, (ACP) Mussa Taibu ambaye aliweka wazi kuwa wamejipanga na kuimarisha usalama.

''Tumejipanga na vikosi vyetu kama kawaida kuhakikisha tunaimarisha usalama wetu na tunahakikisha maeneo yote yana usalama wa kutosha na sio wka hili tu, muda wote vikosi vyetu vipo tayari'', amesema Kamanda Taibu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ubalozi wa Marekani, maeneo yanayohofiwa huenda shambulio likafanyika ni Masaki katika hoteli na migahawa.