
Zoezi la kurejesha fomu za kuwania nafasi ya udiwani na ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM leo limefikia tamati ambapo kati ya waliorejesha fomu hizo jijini Dar es Salaam, yupo Meya wa Manispaa ya Ilala, mstahiki Jerry Silaa.
Silaa, ametangaza kuachana na nafasi ya Umeya na kuelekeza nguvu zake katika ubunge ambao amedai utampa fursa ya kusimamia mafanikio ambayo manispaa ya Ilala imeyapata ikiwa ni pamoja na kuwa manispaa inayoongoza katika ujenzi wa maabara za shule za sekondari, usimamizi wa miradi ya maji na ujenzi wa barabara.
Wakati huohuo, kinyang'anyiro cha kuwania ubunge katika jimbo la Kawe ambalo kwa sasa linashikiliwa na Halima Mdee wa Chadema kimeshika kasi ambapo Katibu wa CCM wilaya ya Kinondoni, Athuman Shesha, amesema jumla ya wana CCM 20 wamejitokeza kuwania kiti hicho.
Kati ya walirejesha fomu katika ofisi za CCM wilaya ya Kinondoni yumo kijana Stanslaus Maganga, anayetajwa kuwa ndiye mtu mwenye umri mdogo kabisa kugombea nafasi ya ubunge nchini kwa sasa akiwa na umri wa miaka 26 tu.
Jumla ya wagombea 105 wamejitokeza kuwania ubunge katika majimbo 9 ya jiji la Dar es salaam wengi wao wakiwa vijana.