Jumapili , 13th Oct , 2019

Daraja la Mto Mnyuzi lililopo Kijiji cha Jitengeni, Kata ya Segera lililopo katikati ya mpaka wa Wilaya ya Korogwe na Handeni mkoani Tanga limekatika kufuatia mvua zilizonesha mfululizo na kusababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya abiria wanaotoka Arusha kwenda Tanga na Arusha kwenda

Dar es salaam baada ya maji kujaa kupita kiasi katika barabara hiyo.

Mvua hizo pia zilisababisha vifo vya watu saba waliosombwa na maji yanayotokana na mafuriko ya mvua.

Tokea jana saa tano asubuhi magari kutoka Arusha kwenda Tanga na Arusha Dar es salaam, yamelazimika kupiga kambi katika eneo hilo wakisubiria msaada wa namna gani daraja hilo litaweza kujengwa ili kuruhusu mawasiliano.

EATV na EA Radio Digital ilifanikiwa kufika katika eneo hilo na kufanya mahojiano na abiria waliokwama kwenye eneo hilo ambapo walilalamika kuhusu gharama kuwa kubwa kutokana na chakula pamoja na huduma za kijamii kuwa juu kupita kiasi na kushindwa kumudu gharama hizo.

''Tunaomba serikali ifanye jitihada za makusudi za kusaidia eneo hili liweze kupitika tunapata adha kubwa sana kwani tokea jana saa tano asubuhi  tupo kwenye eneo hili na watoto wadogo vyakula hatuna na bei za hapa hatuzimudu,''amesema Amani Bakari ambaye ni mmoja wa abiria.

Kwa upande wao madereva waliokwama katika eneo hilo wameiomba serikali kuangalia namna ya kutatufa njia ya sahihi ya kukomesha tatizo hilo kwani siyo mara ya kwanza kujaa maji katika daraja hilo ambapo walisema hali hiyo inahatarisha sana maisha ya wananchi.

Wakazi wa kijiji hicho nao wameiomba serikali kutafuta njia ya kumuokoa mzee mmoja aliyepanda juu ya mti wa muembe kwajili ya kujiokoa tokea jana ambapo alipiga simu na kuomba msaada huo baada ya mafuriko kulikumba eneo alilokuwepo huku mifugo yake ikisombwa na maji.