Jumamosi , 30th Mei , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli , amewataka wakulima kuacha mara moja kuuza mazao yao kwa bei nafuu kwa kuwa huenda mwaka huu au ujao, hali inaweza isiwe nzuri kwani nchi nyingi za Afrika zitakumbwa na shida ya chakula kwa sababu walijifungia ndani kuogopa Corona.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli.

Rais Magufuli ameyabainisha hayo leo Mei 30, 2020, jijini Dodoma, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Ikulu ya Chamwino yenye ukubwa wa Hekari 8,473, na kusisitiza kuwa endapo wataamua kuuza, basi wauze kwa bei ya juu zaidi ili waweze kuiona faida ya nguvu zao.

"Niwaombe ndugu zangu wakulima tujihadhari kuuza mazao yetu kwa bei ya chini, inawezekana mwaka huu au unaokuja usiwe mzuri sana, msiuze vyakula kwa bei ya kutupa mtanunua chakula hicho kwa bei ya juu, na maeneo mengi ya Afrika na katika Dunia yatapata shida ya chakula kwa sababu waliji-lockdown wakati sisi tunalima na kama mtauza uzeni kwa bei ya juu sana, watwangeni sana" amesema Rais Magufuli. 

Aidha Rais Magufuli ameendelea kusisitiza kuwa, kwa sasa Tanzania ni mahali salama baada ya Mwenyezi Mungu kuikoa na janga la Corona.