Jumapili , 22nd Sep , 2019

Rais Dkt John Pombe Magufuli, amemuomba Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Biswalo Mganga, kama sheria itaruhusu akutane na wafungwa wenye makosa ya uhujumu uchumi waliokaa muda mrefu mahabusu, ambao pia wapo tayari komba radhi, na waweze kuzirudisha pesa hizo.

Rais Magufuli amesema hayo leo Septemba 22, 2019, mara baada ya kuwaapisha Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Mkuu, Ikulu jijini Dar es Salaam.

"Kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi  kama wapo watu ambao wanakesi za uhujumu uchumi, utakatishaji wa pesa na wako Mahabusu, na kesi zao hazitawafanya watoke mapema, ila wapo radhi kuzirudisha hizo pesa na kutubu, mimi nashauri sheria ikiruhusu naomba watoke'' amesema Rais Magufuli.

Aidha wakati huo huo Rais Magufuli ameeleza sababu iliyomfanya amtengue Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Stephen Kebwe, kuwa alishindwa kusimamia mkoa wake.

"Ukishaona Mkuu wa Mkoa yupo pale unajua 'automatically' ameshindwa kuhimili Mkoa wake, ukishaona Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wanagombana kisa maslahi na Mkuu wa Mkoa hujawahi hata kufika kukemea maana yake hautoshi" amesema Rais Mgufuli.