Jumatatu , 19th Aug , 2019

Kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili Mwandishi wa habari za Uchunguzi Erick Kabendera,  leo Agosti 19 imepigwa kalenda  hadi Agosti 30 mara baada ya upande wa Serikali kusema haujakamilisha upelelezi.

Mwandishi wa habari za Uchunguzi Erick Kabendera (Mwenye shati la drafti)

Ikumbukwe kuwa awali kesi iliyokuwa inatakiwa kusikilizwa ni ya kuomba dhamana, iliyokuwa imewasilishwa mahakamani hapo na mawakili wa Mtandao wa watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC).

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Wankyo Simon ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa,  upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwandishi wa kujitegemea wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera bado haujakamilika.

Kabendera anashtakiwa kwa Makosa matatu ikiwemo kukwepa Kodi kiasi cha Tsh. Milioni 173,247,047.02, Utakatishaji Fedha na kujihusisha na genge la uhalifu, makosa ambayo yote hayana dhamana.

Erick Kabendera alikamatwa nyumbani kwake maeneo ya Mbweni Dar es Salaam, siku ya Julai 29, 2019, na alihojiwa na vyombo kadhaa vya ulinzi na usalama likiwemo Jeshi la Polisi pamoja na Idara ya Uhamiaji.