Jumanne , 22nd Mei , 2018

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mjini Magharibi Visiwani Zanzibar, Hassan Nassir Ali, amefunguka juu ya uhamisho wake aliopewa siku chache baada ya kuwaonya wanaume juu ya tabia zao zisizofaa kwenye jamii.

Akizungumza na www.eatv.tv, Kamanda Hassan amesema kwamba uhamisho wake ni wa kawaida na wala haujatokana na kauli alizotoa, ambazo zilizua gumzo kwenye mitandao ya kijamii.

Akiendelea kutolea ufafanuzi suala hilo Kamanda Hassan amesema kwamba kauli hiyo aliitoa na alikuwa anamaanisha, lakini haijaleta mtafaruku wowote kwenye jamii kama ambavyo inasemekana, na hata walipoijadili kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar ilikuwa ni utani.

“IGP amesema mwenyewe amefanya uhamisho na uteuzi huu ili kuimarisha safu yake kiutendaji, mimi ningekuwa nimesema nimewakwaza watu sio kweli, hata wale waliosema katika Baraza la Uwakilishi ilikuwa ni kwa utani, ni uhamisho wa kawaida kabisa, wala sio chuki”, amesema Kamanda Hassan.

Kamanda Hassan ameendelea kwa kuwataka wananchi wa Kaskazini Pemba ambako amehamishiwa kufuata sheria bila shuruti kwani kazi iko pale pale.

“Nitaendelea kufanya kazi yangu vizuri nitaendelea kusimamia sheria vizuri, kazi iko pale pale bado mimi ni Kamanda wa polisi nitasimamia sheria za nchi, wala sio jambo langu hili wala mie sio mzee wa vikohozi, mimi nimetoa mifano, hivyo kazi iko pale pale”, amesema Kamanda Hassan.

Kamanda huyo ambaye metokea visiwani Zanzibar wiki iliyopita aliibua mzozo kwenye mitandao baada ya kuwaonya wanaume wenye tabia ya kukohoa pindi waonapo wanawake wenye maumbile makubwa, akisema hilo ni kosa kisheria ambalo linatambulika kama shambulio la aibu.