Jumapili , 13th Oct , 2019

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kuwakamata na kuwafungulia mashataka watu wanaowapotosha wananchi kutokujitokeza kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Mhe. Kangi Lugola

Lugola amesema watu hao wanawarubuni wananchi kwa njia za mitandao ya kijamii, kuwafuata majumbani kwao, wakiwapotosha kususia uchaguzi huo pamoja na kuwadanganya kuwa walishajiandikisha kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, hivyo watatumia vitambulisho hivyo hivyo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 24, 2019.

Akizungumza na wananchi Jimboni kwake Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, mara baada ya kujiandikisha katika kituo cha Sokoni, Kata ya Kibara, Lugola amesema viongozi wa Serikali ya Kijiji pamoja na vyanzo mbalimbali alivyopewa na wananchi mbalimbali, kuna kundi la wananchi wanapita mitaani kuwapotosha wananchi na pia kuwatisha wasifike vituoni kujiandikisha wakiwa na lengo la kuvuruga uchaguzi.

Lugola ameongeza kuwa Wizara yake inalinda amani katika uchaguzi huo, hivyo haiwezi kukaa kimya kuwaacha wapotoshaji hao wakiendelea kuharibu na kutamba mitaa jambo ambalo Serikali ya awamu ya tano kamwe haitakaa kimya.

Pia Waziri Lugola amesema kupitia uchaguzi huo, viongozi wa vijiji na mitaa watasaidia Wizara yake baada ya kuwapata viongozi hao ambao pia wataunda Kamati ya ulinzi na usalama ya Kijiji. Waziri Lugola tayari amejiandikisha katika Kijiji hicho na kupongezwa na wananchi ambao wengi wao walijitokeza baada ya kumuona Mbunge wao akijiandikisha katika kituo hicho.