Katavi : Mbaroni sababu ya vyeti feki

Alhamisi , 7th Nov , 2019

Mtumishi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, Deodatus Jabir (46), anatarajiwa kupandishwa kizimbani kwa makosa ya kughushi cheti cha Udereva kutoka chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), pamoja na kutoa nyaraka za uongo ili kujipatia ajira.

Akitoa taarifa hiyo Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mkoani Katavi, Christopher Nakua, amesema Deodatus alitenda kosa hilo mwaka 2009, kwa kuwasilisha cheti hicho kwa mwajiri wake, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa na kufanikiwa kujipatia ajira huku akijua hajasoma elimu yeyote.

"Kosa lililofanywa na mtumishi huyo wa Halmashauri ni kujipatia ajira kwa kutumia nyaraka za kughushi ni kinyume na vifungu vya 333, 335,337,na 342 vya sheria ya kanuni na adhabu sura ya 16 (toleo la 2002)" amesema Nakua.

Aidha TAKUKURU inatoa wito kwa watumishi wa umma na jamii kwa ujumla, kutojihusisha na vitendo vya kijinai kama kuwasilisha nyaraka za uongo ili kujipatia ajira au kwa manufaa yoyote ambayo ni kinyume na sheria.